Wema na wasanii wenzake washikiliwa kwa tuhuma za mihadarati Tanzania
Polisi nchini Tanzania inawashikilia zaidi ya watu 10 wakiwemo wasanii maarufu na polisi waliotuhumiwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Miongoni mwa watu hao wanaohojiwa yupo msaani maarufu na miss Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu, aliyeitikia wito wa polisi pamoja wasanii wenzake kufika kwa mahojiano.
Hapo jana mkuu wa Mkoa huo wa Dar es Salaam nchini humo, Paul Makonda aliwataja watuhumiwa kadhaa wakiwemo polisi na wasanii kuhusika na biashara hiyo na kuwataka leo kuwaripoti kituo cha polisi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Simon Sirro amesema operesheni ya kuwakamata watu hao ilianza tangu jana ambapo watu watano walitiwa korokoroni na kufikisha idadi ya watu waliokamatwa hadi leo kufikia 17.
Kamanda Sirro amesema kwa sasa imeundwa timu maalum inayowahusisha polisi na vyombo vingine vya usalamaya ili kuendelea kuwatafuta wafanya biashara wa madawa hayo.
Biashara ya madawa ya kulevya ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili nchi ya Tanzania ambapo baadhi wamekuwa wakiinyooshea kidole serikali kwamba hajaichukua hatua kali ya kukabiliana na tatizo hilo.

Favicon Wema na wasanii wenzake washikiliwa kwa tuhuma za mihadarati Tanzania