Kiongozi wa waasi na aliyekuwa Makamu wa rais nchini Sudan Kusini Riek Machar ametangaza vita vipya dhidi ya serikali ya Juba akiwa nje ya nchi.

Machar ambaye yupo jijini Khartoum katika nchi jirani ya Sudan, amesema lengo lake la kutangaza vita ni kutaka kurejea kwa amani, uhuru, demokrasia na utii wa sheria katika nchi yake.

Aidha, ametaka kutumwa haraka kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa la wanajeshi 4,000 lakini pia Jumuiya ya Kimataifa kutoitambua serikali ya rais Salva Kiir.

Machar aliyeikimbia nchi yake mwezi Julai, baada ya kuzuka kwa vita vipya jijini Juba, amemwelezea rais Kiir kama dikteta.

Wachambuzi wa maswala ya Sudan Kusini wanasema, tangazo hili la Machar lilitarajiwa.

“Hatua hii ya Machar kutangaza vita ilitarajiwa, na anataka kuonesha dunia kuwa hawezi kushirikiana na rais Kiir,” alisema Brian Wanyama.

Tangazo hili limekuja wakati huu aliyekuwa Mshirika wa karibu wa Machar, Taban Deng Gai akiendelea kuhudumu kama Makamu wa kwanza wa rais baada ya kiongozi huyo wa waasi kuondoka jijini Juba.

Haijawa wazi ikiwa wapiganaji wa upinzani wa SPLA/IO wanamuunga mkono Machar au Deng.

Machar na washirika wake wa karibuni wamesema hawamtambui Bwana Deng.

Msemaji wa kundi la upinzani lililosalia jijini Juba, John Clement Kuc, amepuuzilia mbali tangazo la Machar na kumtaja kama mtu asiyetaka amani.

Favicon Riek Machar atangaza vita dhidi ya serikali ya Juba