Burundi imewapiga marufuku wachunguzi watatu wa Umoja wa Mataifa baada yao kuchapisha ripoti wakiituhumu serikali kwa kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.

Wachunguzi hao, kwenye ripoti mwezi jana, walisema maelfu ya watu waliteswa, wakanyanyaswa kingono au wakatoweka wakati wa machafuko ya kisiasa yaliyotokea tangu Aprili mwaka jana.

Aidha, walitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mauaji ya halaiki kutokana na kuongezeka kwa machafuko.

Uamuzi huo wa Burundi umetokea siku chache baada ya taifa hilo kutangaza kuwa litajiondoa kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

 

Barua iliyotiwa saini na waziri wa mambo ya nje wa Burundi Alain Aime Nyamitwe ilisema Pablo de Greiff anayetoka Colombia, Christof Heyns kutoka Afrika Kusini na Maya Sahli-Fadel wa Algeria hawatakikani tena Burundi.

Ripoti waliyokuwa wamechapisha walisema kuna « ushahidi mwingi wa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu » ambao kuna uwezekano ukawa ni uhalifu dhidi ya binadamu, na ambao umetekelezwa na serikali ya Burundi na watu wanaoiunga mkono.

Burundi yapiga marufuku wachunguzi watatu wa UN

Lakini akiongea mjini New York Jumatatu, msemaji wa UN Stephane Dujarric aliihimiza Burundi kuendelea kushirikiana na wachunguzi wa umoja huo.

Tangazo kwamba Burundi itajiondoa kutoka mahakama ya ICC lilitolewa wiki iliyopita miezi sita baada ya mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi kusema ingechunguza ghasia zinazoendelea nchini humo.

Umoja wa Afrika (AU) mara kwa mara umeituhumu mahakama hiyo kwa kuwabagua Waafrika.

Favicon Burundi yapiga marufuku wachunguzi watatu wa UN